KIMATAIFA
Polisi amuua mwenzake kwa kumpiga risasi na yeye ajiua baada ya mechi
Polisi huko nchini Kenya, amemuua mwenzake kwa kumpiga risasi usiku wa kuamkia leo na yeye amejiua baada kutazama mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kati ya Manchester City na Monaco.
Kabla ya polisi huyo, Konstebo Constable Patrick Kihagi kujiua kwa kujipiga risasi kichwani, alimjeruhi polisi mwingine kwa kumpiga risasi begani.
Polisi aliyekufa ametajwa kwa jina la Konstebo James Makokha, na kabla ya kifo alikuwa akifanya kazi Jogoo House. Inadaiwa kuwa Makokha alipigwa risasi wakati akitaka kumaliza ubishani kati ya Kihagi na Ng’etich.
Kabla ya tukio hilo saa saba na nusu usiku kwenye eneo la Tassia, Nairobi nchini Kenya, polisi hao watatu walikuwa baa wakitazama mpira na kisha wakaanza kubishana, wakatoka nje. Mashuhuda wanadai kuwa, walipotoka nje walizidi kubishana, Kihagi akatoa bastola na kumjeruhi mwenzake, Konstebo Dominic Ng’etich kwa risasi.
Kihagi alikuwa akifanya kazi katika kituo cha Embakasi, Ng’etich anafanya kazi kwenye kituo cha polisi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
0 comments