KIMATAIFA
Amnesty International yatahadharisha kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Marekani
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetahadharisha kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika katika bara la America.
Katika taarifa yake ya kila mwaka iliyotolewa leo kuhusu hali ya haki za binadamu kwenye mabara matano ya dunia, Amnesty International imesema kuwa, ukiukwaji wa haki za binadamu katika baadhi ya nchi za bara America hususan dhidi ya wakazi asilia, wanawake, wasichana na waandishi wa habari umeongezeka katika mwaka uliopita wa 2016.
Kesi nyingi zaidi za ukiukaji wa haki za binadamu katika ripoti hiyo zimesajiliwa nchini Marekani ikiwa ni pamoja na vifungo vya siri vya shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA na mienendo mibaya na ya kikatili katika jela ya Guantanamo.
Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, kuna wasiwasi kuhusu mienendo ya kikatili dhidi ya wahajiri na wakimbizi na vilevile katika jela za federali na za majimbo ya Marekani na mienendo mibaya ya polisi.
Amnesty International pia imetahadharisha kuhusu athari mbaya za siasa za kuwapiga vita wahajiri za Rais Donald Trump wa Marekani.
0 comments