KIMATAIFA
Juhudi za majirani wa Libya za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiy
Katika kuendelea juhudi za kieneo kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa sasa wa kisiasa wa Libya, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi jirani na nchi hiyo wamesisitiza upinzani wao dhidi ya kutumika nguvu ya aina yoyote ya kijeshi kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo.
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri, Tunisia na Algeria wamesisitiza juu ya kutatuliwa mgogoro wa Libya kwa njia za kisiasa na kwamba, majirani wa nchi hiyo wanafuatilia ufumbuzi wa ndani wa kisiasa wa mgogoro huo. Abdel Gadir Masahil, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria sambamba na kuashiria kwamba, hatima na mustakabali wa Libya unapaswa kuwa mikononi mwa Walibya wenyewe amesema kuwa, Misri, Algeria na Tunisia zinaunga mkono hatua yoyote ile ya kujiweka mbali na utoaji mashinikizo dhidi ya mazungumzo ya makundi ya Libya. Abdel Gadir Masahil amesema hayo katika mkutano wa pande tatu wa Tunisia, Algeria na Misri uliofanyika huko Tunisia.
Mkutano wa Tunisia ni mwenendelezo wa utekelezaji wa mpango wa Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo wenye lengo la kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa wa pande zote mgogoro wa Libya. Aidha mkutano wa Mawaziri hao wa Mashauri ya Kigeni umeelezwa kuwa ni utangulizi wa mkutano wa viongozi wa nchi hizo tatu utakaofanyika hapo baadaye. Libya ilitumbukia katika vurugu na machafuko tangu mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Kutokana na uingiliaji wa kijeshi wa baadhi ya madola makubwa katika masuala ya ndani ya Libya hususan Shirika la Kijeshi la NATO, nchi hiyo imeendelea kushuhudia vurugu, machafuko na ukosefu wa amani na usalama.
Hata kama hadi sasa kumefanyika juhudi kubwa za kieneo na kimataifa kwa ajili ya kufikia ufumbuzi wa mgogoro wa Libya, lakini juhudi hizo hazijawa na natija kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutoshiriki makundi yote ya kisiasa au kutaka hisa nchi mbalimbali katika kadhia ya Libya.
Hata hivyo kuendelea hali hii na mazingira ya sasa ya Libya yamedhuru mafanikio ya nchi nyingine pia za eneo hilo. Uhajiri haramu kuelekea Libya na kugeuzwa nchi hiyo kama kivuko cha kupita wahajiri wanaokimbilia barani Ulaya, kuweko makundi ya kigaidi na kuingia na kutoka kwao katika mipaka ya nchi hiyo na kuelekea katika nchi nyingine jirani, ni matatizo makubwa kabisa kwa sasa yanayoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Akthari ya makundi ya kigaidi yameingia nchini Tunisia, Algeria na nchi nyingine jirani yakitokea Libya na kuvuruga amani na uthabiti wa nchi hizo. Hii ni katika hali ambayo, nchi hizo zenyewe zinakabiliwa na matatizo ya ndani. Tunisia ingali inakabiliwa na tatizo la uchumi na ukosefu wa usalama na bila shaka kuongezeka makundi ya kigaidi nchini humo kunaweza kupunguza kipato cha nchi hiyo kinachotokana na sekta ya utalii.
Misri nayo inapitia kipindi kigumu cha mizozo ya kisiasa ikijipapatua ili kufikia uthabiti. Nchini Algeria hata kama mazingira ya nchi hiyo ni mazuri ikilinghanishwa na nchi zilizotajwa, lakini wasiwasi wa kuenea ugaidi na kuweko magaidi katika mipaka na ardhi ya nchi hiyo ni tishio kubwa kwa sasa. Katika upande mwingine, mgogoro wa sasa wa Libya umeandaa mazingira ya uingiliaji wa madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Baadhi ya nchi za Magharibi zinataka kuweko kijeshi nchini Libya na kwa muktadha huo, kutumia nafasi ya nchi hiyo pamoja na vyanzo vya utajiri ilivyonavyo kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa.
Aidha baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo nazo, zinachochea moto wa hitilafu za kisiasa na kuifanya Libya ibakie katika hali hii hii ya mgogoro na ndio maana zinaendelea kusukuma mbele gurudumu la siasa zao za uingiliaji masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Ukweli wa mambo ni kuwa, matatizo ya sasa ya Libya yamezishughulisha pia nchi zinazopakana na nchi hiyo kiasi kwamba, kwa mara nyingine tena nchi hizo zimesisitiza kuwa, zinapinga uingiliaji wa kijeshi katika nchi hiyo. Na ndio maana kwa sasa zinafanya kadiri ziwezavyo ili kuikwamua Libya na mgogoro inaokabiliwa nao. Hata hivyo wajuzi wa mambo wanaamini kwamba, juhudi hizo zitakuwa na matunda pale tu zitakapokuwa hazina malengo ya kutaka hisa na wakati huo huo, makundi ya Libya yawe na ushiriki amilifu bila kusahau suala la kuweko azma ya kweli ya kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo
0 comments