KIMATAIFA
Democrats: Tutaanzisha mchakato wa kumg'oa madarakani Trump
Wabunge na wanasiasa wa chama cha Democrat nchini Marekani wanasema mienendo ya Rais wa nchi hiyo Donald Trump katika muda wa wiki tatu zilizopita imeibua uwezekano kuanzishwa mchakato wa kumng'oa mamlakani rais huyo.
Katika mahojiano na shirika la habari la CNN jana usiku, Mwakilishi wa Minnesota wa chama cha Democrat, Keith Ellision, alisema mienendo ya Trump yakiwemo matamshi yake ya kugongana ni baadhi ya mambo aliyoyafanya rais huyo wa Marekani chini ya mwezi mmoja, ambayo yanatia nguvu hoja ya kuanzishwa mchakato wa kumuondoa ofisini mara moja.
Ellison, ambaye anawania kuwa kinara wa Chama cha Democratic nchini Marekani amesema lengo lao la kuweka wazi suala la kuanzishwa harakati za kumbandua mamlakani Trump limetokana na ukweli kuwa, mfanyabiashara huyo tajiri amekiuka mara kadhaa misingi ya katiba na hivyo hafai kuendelea kuongoza.Amesema kimsingi jambo ambalo limewafanya waanzishe mchakato huo, ni kwa ajili ya kuinusuru hadhi na heshima ya Ofisi ya Rais.
Wiki iliyopita, Kevin Barrett, mchanganuzi wa masuala ya siasa na mwandishi wa habari wa Marekani alisema matamshi ya kukinzana yanayotolewa mara kwa mara na Rais Donald Trump na hususan matamshi aliyoyatoa hivi karibuni dhidi ya Iran yanadhihirisha kuwa bilionea huyo ana matatizo ya kiakili.
Mijadala na minong'ono inaendelea kufanyika katika kona mbali mbali za nchi kuhusu hali ya kiafya ya Trump, baadhi ya wanasaikolijia wakisema kuwa rais huyo wa Marekani anahitaji matibabu ya haraka kabla ya mambo kuharibika zaidi.
0 comments