KIMATAIFA
Mkuu wa shirika la mafuta ateuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Somalia
Rais mpya wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo aliyeapishwa jana mjini Mogadishu amemteua mkurugenzi wa shirika moja la mafuta kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.
Shirika la habari la Reuters limetagaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Hassan Ali Khaire, Mkurugenzi wa Shirika la Mafuta na Gesi la Soma la Uingereza na ambaye pia ana uraia wa Norway, ndiye Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Tovuti ya radio ya serikali ya Muqdisho.net imewataka wananchi wa Somalia kushirikiana na kufanya kazi bega kwa bega na Waziri Mkuu mpya katika mchakato wa kuundwa serikali mpya.
Hata hivyo baadhi ya wadadisi wa mambo wamesema hatua ya Rais Farmaajo ya kumteua mkuu huyo wa shirika la mafuta, huenda ikaibua suala la mgongano wa maslahi.
Mohamed Mubarak, mwanaharakati mashuhuri wa kupambana na ufisadi nchini Somalia amepongeza uteuzi wa Ali Khaire na kusisitiza kuwa, kuja kwa Waziri Mkuu huyu mpya kunamaanisha kuwa nchi hiyo haitashuhudia masuala ya rushwa kwa angalau miaka minne ijayo.
Baada ya kuapishwa katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi wa nchi kadhaa za kanda hiyo chini ya hatua kali za ulinzi, rais mpya wa Somalia ameahidi kurejesha heshima ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika lakini pia akaonya kwamba, itachukua miongo miwili kurekebisha nchi hiyo.
0 comments