KIMATAIFA
Hahakama Kuu Afrika Kusini yazuia serikali kujiondoa mahakama ya ICC
Mahakama Kuu ya Afrika Kusini imezuia zoezi la serikali ya nchi hiyo la kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Hatua hiyo inatambuliwa kuwa ni pigo jingine kubwa kwa Rais Jacob Zima wa nchi hiyo anayeandamwa na kashfa nyingi ikiweno ya ubadhirifu wa mali ya umma.
Hata hivyo Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini, Michael Masutha amesema serikali ya Pretoria itaendeleza mikakati ya kujiondoa kwenye mahakama hiyo yenye makao yake The Hague nchini Uholanzi akiashiria kwamba, hukumu ya Mahakama Kuu ya kuzuia zoezi hilo imetegemea hoja kwamba, uamuzi wa serikali wa kujiondoa katika mahakama ya ICC haukupasishwa na Bunge.
Serikali ya Afrika Kusini ilianza mkakati wa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) Oktoba mwaka jana suala ambalo litaifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza kujiondoa katika mahakama hiyo Oktoba mwaka huu.
Nchi nyingi za Afrika zinaituhumu Mahakama ya ICC kwamba inawaandama tu viongozi wa nchi za bara hilo na kufumbia macho uhalifu na jinai kubwa zinazofanywa na viongozi wa nchi nyingine duniani.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilianzishwa Julai mwaka 2002 na ina nchi wanachama 124 na lengo lake kuu ni kufuatilia wahalifu wa mauaji ya kimbari, jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita.
0 comments