KIMATAIFA
Amri mpya ya Trump yapokelewa kwa mashaka
Rais wa Marekani Donald Trump amesaini amri mpya inayozuia watu kutoka mataifa 6 yenye Waislamu wengi kuingia nchini Marekani, ikiwa ni marekebisho ya amri ya kwanza ambayo ilikwamishwa na maamuzi ya mahakama.
Rais Trump ameisaini amri mpya ya marufuku ya safari, ambayo imeiacha Iraq
Amri hiyo mpya ya Rais iliyosainiwa na Donald Trump ambayo itaanza kutekelezwa tarehe 16 mwezi huu wa Machi, inashikilia marufuku ya siku 90 kwa wasafiri wanaotoka katika mataifa sita yenye waislamu wengi kuingia nchini Marekani. Nchi hizo ni Iran, Libya, Syria, Somalia, Sudan na Yemen. Inawahusu wale tu watakaotaka kupata visa kwa wakati huu, ikiwa na maana kuwa haiwaathiri watu 60,000 ambao tayari wamezipata visa, kama ilivyokuwa kwa amri ya awali.
Iraq ambayo ilikuwa kwenye orodha ya amri ya mwanzo imeondolewa, na kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson, hatua hiyo imetokana na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
''Iraq ni mshirika muhimu katika vita dhidi ya kundi la IS. Mikakati ya uhakiki iliyofanywa mnamo mwezi mmoja uliopita, imeonyesha hatua mbali mbali za kiusalama, ambazo zitaziwezesha serikali ya Iraq na wizara ya mambo ya nje ya Marekani, kutimiza lengo la pamoja, la kuzuia watu wenye malengo ya kigaidi kufika nchini Marekani''. Amesema Tillerson.
Amri ile ile katika kasha mpya
Amri ya kwanza ilisababisha mtafaruku katika viwanja vya ndege vya Marekani
Mawakili wanaohusika na masuala ya uhamiaji wamesema amri hii mpya bado inawalenga waislamu, na haikuweza kuondoa matatizo yaliyosababishwa na amri ya awali. Wataalamu wa masuala ya sheria hata hivyo wametoa hoja kuwa itakuwa vigumu kuipinga mahakamani amri hii, kwa sababu inawalenga watu wachache waishio nchini Marekani, na inatoa nafasi ya kuwalinda.
Wabunge wa chama cha Democratic wamesema amri hii mpya ni ile ile ya awali iliyofungwa upywa, ikiwalenga waislamu na wakimbizi, suala ambalo kiongozi wa wabunge hao Nancy Pelosi amesema ni kinyume cha katiba.
Baadhi ya warepublican ambao walikuwa wakiipinga amri ya kwanza ya Rais Trump wameonekana kuikubali hii mpya.
Huku hayo yakijiri, wabunge wa chama cha Republican wamezindua mpango wao wa bima ya afya, wanaotaka uchukue nafasi ya ule ulioachwa na rais Barack Obama, maarufu kama Obama Care. Mpango huo waliouita American Health Care Act, unaondoa misingi muhimu ya ule wa rais Obama, zikiwemo ruzuku na kodi zinazoambatana nao.
Mpango wa Bima ya Afya wa Rais Obama ulipingwa vikali na Warepublican
Ingawa warepublican wameunadi mpango wao kama suluhisho linaloweka mbele maslahi ya wagonjwa badala ya urasimu, hawakutoa takwimu za gharama wala idadi ya watu watakaonufaika nao.
Hali kadhalika mpango huo mpya umeziacha nguzo mbili kubwa za Obamacare, ambazo ni kuyakataza makampuni ya bima kuwabagua wateja wenye magonjwa yanayojulikana, na kuruhusu bima ya wazazi kuwahudumia watoto wao hadi wafikapo umri wa miaka 26.
Mpango huo utajadiliwa kwanza katika mabaraza mawili ya bunge la Marekani, kabla ya kupelekwa Ikulu ya White House ili usainiwe na Rais Trump kuwa sheria rasmi.
0 comments