Rais wa zamani wa bunge Ulaya Martin Schulz ameteuliwa kukiongoza chama cha Social Demokratik katika jaribio lao la kumuondowa madarakani Kansela Angela Merkel na amesema atapigania kuwapo kwa usawa zaidi na kuondokana na mgawanyiko nchini Ujerumani.
Schulz ameuambia umma wa zaidi ya watu 1,000 katika makao makuu ya chama hicho mjini Berlin Jumapili (29.01.2016 )kwamba atapigania kuwepo kwa taratibu za kodi zitakazozingatia haki zaidi na kuhakikisha kwamba watu walioko katika maeneo ya vijijini wananufaika na mafao sawa na wenzao walioko katika miji mkubwa.
Pia ametowa wito wa kuwepo kwa mshikamano zaidi barani Ulaya katika suala la uhamiaji na kuvielezea vitendo vya Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban kuwa ni "tusi" kwa Umoja wa Ulaya.
Shulz amesema atavitaka vyama vyote kufikia makubaliano kuzuwiya aina ya kejeli zilozokuwa zimeshuhudiwa wakati wa kampeni za uchahuzi wa rais nchini Marekani mwaka jana.